Matthew 13

Mfano Wa Mpanzi

(Marko 4:1-9; Luka 8:4-8)

1 aSiku iyo hiyo Isa akatoka nje ya nyumba, akaketi kando ya bahari. 2 bUmati mkubwa mno wa watu ukakusanyika kumzunguka, hata ikabidi aingie katika chombo na kuketi humo, nao watu wote wakawa wamesimama ukingoni mwa bahari. 3 cNdipo akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. 4Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila. 5Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba. 6Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina. 7Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea. 8 dMbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri ambapo zilitoa mazao, nyingine mara mia moja, nyingine mara sitini, na nyingine mara thelathini. 9 eMwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

Sababu Ya Kufundisha Kwa Mifano

(Marko 4:10-12; Luka 8:9-10)

10Wanafunzi wake wakamwendea, wakamuuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?”

11 fAkawajibu, “Ninyi mmepewa kuzifahamu siri za Ufalme wa Mbinguni, lakini wao hawajapewa. 12 gKwa maana yule aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. 13 hHii ndiyo sababu nasema nao kwa mifano: “Ingawa wanatazama, hawaoni;
wanasikiliza, lakini hawasikii, wala hawaelewi.

14 iKwao unatimia ule unabii wa Isaya aliposema: “ ‘Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa;
na pia mtatazama lakini hamtaona.

15 jKwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu;
hawasikii kwa masikio yao,
na wamefumba macho yao.
Wasije wakaona kwa macho yao,
na wakasikiliza kwa masikio yao,
wakaelewa kwa mioyo yao,
na kugeuka nami nikawaponya.’

16 kLakini heri macho yenu kwa sababu yanaona, na heri masikio yenu kwa sababu yanasikia. 17 lAmin, nawaambia, manabii wengi na wenye haki walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.

Maelezo Ya Mfano Wa Mbegu

(Marko 4:13-20; Luka 8:11-15)

18 m“Sikilizeni basi maana ya ule mfano wa mpanzi: 19 nMtu yeyote anaposikia neno la Ufalme naye asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. Hii ndiyo ile mbegu iliyopandwa kando ya njia. 20 oIle mbegu iliyopandwa kwenye sehemu yenye mawe ni mtu yule ambaye hulisikia neno na mara hulipokea kwa furaha. 21 pLakini kwa kuwa hana mizizi yenye kina ndani yake, lile neno hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, yeye mara huchukizwa. 22 qIle mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu alisikiaye neno, lakini masumbufu ya maisha haya na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda. 23 rLakini ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri ni yule mtu ambaye hulisikia neno na kulielewa. Naye hakika huzaa matunda, akizaa mara mia, au mara sitini, au mara thelathini ya mbegu iliyopandwa.”

Mfano Wa Magugu

24 sIsa akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. 25Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. 26Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea.

27“Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’

28“Akawajibu, ‘Adui ndiye alifanya jambo hili.’

“Wale watumishi wakamuuliza, ‘Je, unataka twende tukayang’oe?’

29“Lakini akasema, ‘Hapana, msiyang’oe, kwa maana wakati mking’oa magugu mnaweza mkang’oa na ngano pamoja nayo. 30 tAcheni ngano na magugu vikue vyote pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto; kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ”

Mfano Wa Mbegu Ya Haradali

(Marko 4:30-32; Luka 13:18-19)

31 uAkawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa Mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua, akaipanda shambani mwake. 32 vIngawa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua ni mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, nao huwa mti mkubwa, hadi ndege wa angani wanakuja na kutengeneza viota katika matawi yake.”

Mfano Wa Chachu

(Luka 13:20-21)

33 wAkawaambia mfano mwingine, “Ufalme wa Mbinguni unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga mpaka wote ukaumuka.”

Sababu Ya Isa Kutumia Mifano

(Marko 4:33-34)

34 xIsa alinena mambo haya yote kwa makutano kwa mifano. Wala hakuwaambia lolote pasipo mfano. 35 yHii ilikuwa ili kutimiza lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii aliposema: “Nitafungua kinywa changu niseme nao kwa mifano;
nitahubiri mambo yaliyofichika
tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.”

Ufafanuzi Wa Mfano Wa Magugu

36 zKisha Isa akaagana na makutano, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.”

37 aaAkawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu. 38 abShamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa Ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. 39 acYule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika.

40 ad“Kama vile magugu yang’olewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. 41 aeMwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka Ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. 42 afNao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. 43 agNdipo wenye haki watang’aa kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.

Mfano Wa Hazina Iliyofichwa Na Lulu

44 ah“Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.”

45 ai“Tena, Ufalme wa Mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. 46 ajAlipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua.”

Mfano Wa Wavu

47 ak“Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. 48Ulipojaa, wavuvi wakavuta pwani, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa. 49 alHivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. 50 amNao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”

51Isa akauliza, “Je, mmeyaelewa haya yote?”

Wakamjibu, “Ndiyo.”

52 anAkawaambia, “Basi kila mwalimu wa sheria aliyefundishwa elimu ya Ufalme wa Mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka ghala yake mali mpya na mali ya zamani.”

Isa Akataliwa Nasiri

(Marko 6:1-6; Luka 4:16-30)

53 aoIsa alipomaliza kutoa mifano hii, akaondoka. 54 apAlipofika mji wa kwao, akawafundisha watu katika sinagogi lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza?” 55 aq“Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si yeye aitwaye Mariamu, nao ndugu zake si Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda? 56 arNao dada zake wote, hawako hapa pamoja nasi? Mtu huyu amepata wapi basi mambo haya yote?” 57 asWakachukizwa naye.

Lakini Isa akawaambia, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani kwake.”

58 atNaye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.
Copyright information for SwhKC